KCSE ONLINE

Esoma Online Revision Resources

Kuandika - Kiswahili Kidato Cha 2

Kufikia mwisho wa somo hili, unapaswa kuwa na uwezo wa:
i) kueleza maana ya muhtasari
ii) kueleza umuhimu wa muhtasari
iii) kufafanua hatua za kuzingatia uandikapo muhtasari
iv) kuandika muhtasari wa kifungu.


MUHTASARI

Muhtasari ni ufupisho wa habari bila kupoteza maana iliyokusudiwa.
Muhtasari huwezesha mtu kutoa habari ndefu kwa maneno machache na kwa muda mfupi ili kurahisisha mawasiliano.Ufupisho una manufaa mengi katika shughuli za kila siku.
Hutumiwa hususan katika mawasiliano na matangazo
mbalimbali kama vile ya kibiashara na vifo, uandishi wa habari na makala ya magazeti, uandishi wa ripoti na kumbukumbu, maandalizi ya mitihani,uandishi wa arafa.


Ufupisho husaidia kutumia wakati vyema na pia kuokoa fedha na rasilimali.
Ujuzi wa kuandika muhtasari ni jambo la lazima maishani. 

Hatua za kuzingatiwa katika kuandika muhtasari
i) kusoma na kuelewa makala.
ii) kuchagua au kuteua mambo muhimu au kiini cha habari huku tukijiepusha na maelezo ya ziada, mifano, vielezi au tamathali za usemi.
iii) Palipo na orodha ya mambo au vitu, ni muhimu kutumia maneno ya kijumla.
iv) kuandika kwa mtiririko mambo muhimu tuliyoyateua kwa hati nadhifu.Ufupisho wa hotuba

Sikiliza kwa makini hotuba zifuatazo
 

Hotuba A
Wananchi hamjambo! Hamjambo tena. Na baada ya salamu hizi, nimesimama mbele yenu kuwasalimia. Jambo lingine nimekuja kwenu leo kuwaomba kura zenu. Ninataka niwe mwakilishi wenu katika eneo hili la bunge
 

Hotuba B
Wananchi hamjambo, niko hapa kuwaomba kura ili niwe mbunge wenu.
Hotuba ya kwanza ina maneno mengi kuliko ya pili lakini ujumbe ni uleule.

Soma kifungu kifuatacho kisha


Visa vya utapeli vinaendelea kuongezeka humu nchini kwa kasi mno. Wananchi wengi wametapeliwa kiasi kikubwa cha pesa na watu ambao hujidai kuweza kutatua matatizo waliyo nayo. Idadi kubwa ya vijana wameingia katika mtego huu wanaposhawishiwa kwa kupewa ahadi za ajira ambayo imekuwa nadra kupatikana. Wengine ni wananchi wanaotafuta nyumba za kukodisha au viwanja vya kujengea. Hawa hutapeliwa na mawakala ambao hujifanya wanawakilisha mashirika fulani. Mawakala hawa huchukua pesa na kutoroka. Inasikitisha kuwa matapeli wengine wanatumia dini. Wao huwadanganya watu kuwa, wakipewa pesa na kuziombea zitaongezeka maradufu, jambo ambalo haliwezekani.

Ili kukabiliana na tatizo hili, ni muhimu kwa wananchi kuwa makini zaidi wanapojihusisha na watu wasiowafahamu vyema. Vijana wanaotafuta ajira wanapaswa kuwajibika, kuchunguza vizuri ili kubaini mashirika yanayotangaza kazi yapo au ni ya kufikiria tu. Serikali inaweza kusaidia katika kuwasaka, kuwanasa na kuwachukulia hatua matapeli. Vile vile vyombo vya habari viangazie visa vya aina hii ili kutahadharisha na kuwawezesha wananchi kuwa makini zaidi.

1. Dondoa hoja muhimu katika aya ya kwanza. (maneno 25)
2. Fupisha aya ya pili.

MAJIBU

1. Visa vya utapeli vimeongeka. Walioathirika ni vijana wanaotafuta ajira, watu wanaotafuta nyumba na viwanja na wale wenye tamaa ya pesa.


2. Ili kutatua tatizo hili, wananchi wanapaswa kumakinika, vijana wanaotafuta kazi wawe na subira na uangalifu, seriksli iwaadhibu wahusika na vyombo vya habari viangazie visa hivi ili watu zaidi wasihadaiwe.

Utungaji wa kiuamilifu
Utungaji wa kiuamilifu ni stadi zinazohusu maarifa na ujuzi wa tungo ambazo mwanafunzi ye yote atahitaji katika maisha yake ya kila siku hata baada ya mafunzo ya shuleni.
Utungaji wa kiuamilifu huwa na taratibu ambazo lazima zifuate.
Maarifa haya yanahusu tungo kama , insha za ripoti, hotuba, barua, kumbukumbu, hojaji, resipe, shajara na kadhalika.

Kufikia mwisho wa kipindi hiki, unatakiwa uwe na uwezo wa:
i) kueleza maana ya tungo za kiuamilifu
ii) kufafanua maana ya hotuba
iii) kubainisha umuhimu wa hotuba
iv) kueleza muundo wa hotuba
v) kuandika hotuba ipasavyo

Hotuba

Hotuba ni taarifa inayotolewa na mtu mbele ya hadhira kwa nia ya kuwasilisha ujumbe mahususi, kutoa msimamo au kuelekeza.


Muundo wa hotuba huwa na sehemu tatu.
Sehemu ya kwanza ni ya utangulizi ambao ndio mwanzo wa hotuba. Utangulizi hushirikisha kuwatambua wale waliohudhuria.Utambulishaji huu,hufanywa kwa kutaja wadhifa wa juu. Vile vile ni katika utangulizi ambapo maamkuzi hufanywa.


Utangulizi hufuata na mwili ambao ndio kiini cha hotuba yenyewe. Mhutubi huelezea mada, kiini ,mapendekezo au ushauri wake.


Hotuba hukamilika kwa hitimisho ambapo mhutubi hutoa shukrani zake na kuagana na hadhira yake.

Tazama video hii na usikilize kwa makini.je umeona na kusikia nini?


Katika video kuna hadhira. Mbele ya hadhira, kuna mtu anayezungumza. Aliyesimama mbele ya umati anatoa hotuba.


Hotuba aghalabu huweza kupitisha ujumbe ili kuelimisha, kushawishi, kushauri, kutahadharisha na kuhimiza
.Ujumbe wa hotuba hutegemea muktadha husika.

Tazama na kusikiliza video hizi mbili.


Wahutubi hawa wana tofauti zipi katika hotuba zao?
Inadhihirika kwamba mhutubi wa kwanza ni bora kuliko wa pili.Hatibu bora anapaswa kuwa na sifa zifuatazo:


i) ana ukakamavu
ii) sauti nzuri na inayosikika vizuri
iii) anatumia viziada lugha kama vile masaja,ishara za mikono na kadhalika.
iv) anahusisha hadhira yake kikamilifu
v) hutumia lugha fasaha na ya adabu
vi) ana mawazo yaliyopangwa kimantiki
vii) anatumia lugha ya kusisimua na kuteka urazini wa hadhira
viii) hajirudii bila sababu
ix) ana uwezo wa kushawishi na kuhamasisha hadhira
x) kuelewa hadhira yake vilivyo

Umealikwa kama mgeni wa heshima katika hafla ya siku ya vijana.
Andika hotuba ukayoitoa kuhusu nafasi na majukumu la vijana katika jamii,
changamoto zinazowakabili vijana, namna vijana wanaweza kuimarisha maisha yao
na ya wakenya wengi.

Kufikia mwisho wa kipindi hiki unatakiwa uwe na uwezo wa:
i) kueleza maana ya Resipe
ii) kueleza umuhimu wa Resipe
iii) kueleza muundo wa Resipe
iv) kutambua msamiati wa mapishi mbalimbali
v) kuandika Resipe

Resipe ni maelezo ya namna ya kutayarisha chakula mahususi.Hushirikisha orodha ya viungo na kiasi kinachohitajika kwa vyakula hivyo kutegemea idadi ya walaji. Resipe hutegemea walaji mathlaani watoto, wazee, wagonjwa, wachezaji, wajawazito na kadhalika.

RESIPE YA KITOWEO CHA KUKU


Kulingana na video uliyoitazama umetambua wazi kwamba utayarishaji wa kitoweo cha kuku hufuata utaratibu ufatao:

Mahitaji

1. Idadi ya walaji 4.
2. Vinavyohitajika na vipimo vyake
i. Kuku 1.
ii. Mafuta ya kukaanga vijiko 2 vikubwa.
iii. Kitunguu maji 1 (kikubwa).
iv. Nyanya 3 mbivu.
v. Chumvi kijiko kidogo.
vi. Bizari iliyosagwa kijiko 1 kidogo.
vii. Pilipili hoho 1.
viii. Maji vikombe vidogo 3
ix. Dania fungu 1
x. Biringanya

3. Utaratibu
  • Osha vipande vya nyama ya kuku,biringanya,dania,pilipili hoho,nyanya na vitunguu
  • Teleka sufuria juu ya moto
  • Chemsha mafuta kwa dakika moja
  • Katakata vitunguu na kuviweka ndani ya mafuta.
  • Vikigeuka rangi kahawia, weka nyanya na pilipili hoho kisha tumbukiza vipande vya nyama ya kuku ndani ya mafuta.
  • Tia chumvi na bizari na kukoroga.
  • Funika kwa dakika 20.
  • Punguza kiwango cho moto kwa dakika 10.
  • Kitoweo kimeiva na chaweza kuandaliwa pamoja na kachumbari na kuliwa kwa sima au wali.

RESIPE YA UGALI

Maelekezo ya kutayarisha

Mahitaji
1. Idadi ya walaji 4
2. Viungo
maji lita 1
unga kilo 1


3. Utaratibu
Chemsha maji hadi yatokote
Weka unga
Koroga mchanganyiko kwa mwiko hadi ushikamane.
Baada ya dakika 5 punguza kiasi cha moto halafu funika.
Epua sufuria kisha tia sima kwenye sahani halafu andaa mlo.

 

RESIPE YA UJI

Jinsi ya kutayarisha

Mahitaji
a) kikombe kimoja cha unga wa wimbi
b) vikombe viwili vya maji
c) sukari
d) kijiko kimoja cha siagi
Utaratibu
a) Tekeleka maji kwenye sufuria hadi yatokote
b) tengeneza mchanganyiko wa unga wa wimbi na maji kwenye bakuli kando
c) mwaga mchanganyiko huo kwenye maji yaliyotokota halafu ukoroge.
d) acha mchanganyiko huo utokote kwa dakika kumi
e)ongeza sukari
f)sasa epua sufuria, na utie uji kwenye vikombe halafu uandae.

UANDISHI WA RESIPE
Tazama vibonzo kwa makini. Umetambua kuwa kuna hatua maalum za kuzingatiwa katika kuandika Resipe?


1. Kuchagua na kutaja aina ya lishe kama vile asusa, ugali, wali, kitoweo na vyakula vinginevyo.
2. Kuonyesha idadi ya walaji.
3. kuandika orodha ya vipimo vya viungo-andika idadi ya vipimo kwa nambari.
4. Kueleza jinsi ya kupika
5. kuandaa

andika resipe ya chapati kwa kitoweo cha maharagwe

UMUHIMU WA RESIPE

i) hutusaidia kutoa lishe bora kwa jamii
ii) husaidia kujua namna ya kupika chakula kizuri
iii) Hutuelekeza katika kujua kiasi cha chakula kwa idadi fulani ya walaji.
iv) Kupitia Resipe, tunajua aina mbalimbali za mapishi kulingana na tamaduni mbalimbali).

Imedhihirika kwamba Resipe ni muhimu kwa kuwa:

i) hutusaidia kutoa lishe bora kwa jamii
ii) husaidia kujua namna ya kupika chakula kizuri
iii) hutuelekeza katika kujua kiasi cha chakula kwa idadi fulani ya walaji.
iv) kupitia Resipe, tunajua aina mbalimbali za mapishi kulingana na tamaduni
mbalimbali.

Utungaji huu hujikita katika uandishi wa kisanaa yaani ufundi na urembo unaotokana na mbinu ya uwasilishaji.
Insha hizi zinahusu jinsi lugha inavyotumiwa.

Kufikia mwisho wa kipindi hiki, unahitajika:
i) kueleza maana ya michezo ya kuigiza
ii) kueleza umuhimu wa michezo ya kuigiza
iii) kufafanua muundo wa mchezo wa kuigiza
iv) kuandika mchezo wa kuigiza ukizingatia kanuni za utungaji ipasavyo


Tazama hii video kwa makini.


i) Umeona nini?
ii) Waigizaji wamevaa vipi?
iii) Wako wapi?
v) Lugha yao inaandamana na nini ?

Huu ni mchezo wa kuigiza. Mchezo unaigizwa jukwaani. Waigizaji huwa na mavazi maalum-maleba yanayooana na nafasi wanazoigiza. Mazungumzo yao yamejaa ishara, hisia na huambatana na utendaji. Aghalabu lugha hii husheheni matumizi ya tamathali za usemi ili kuteka urazini wa hadhiraSoma kisehemu hiki cha mchezo.

(Jukwaani. Ni nyumbani. Baba anaingia jioni. Anamkuta mwanawe anayesomea shule ya bweni nyumbani

Baba : (Akishtuka) Unafanya nini hapa mwanangu?

Mwana: (Akilia) Ni-niki kuambia u- ta-nirudi.

Baba : Kwani umefanya nini?

Mwana : Nilipatikana

Baba : ( kwa ukali)Ulipatikana na nini?

Mwana : na ..na.. na Simu tamba.

Baba : (akimkaribia na kumkaripia)Simu ya nani?

Mwana : ( Huku akitetemeka)Ni..li..pewa na..na.. rafiki yangu na...na.... sikujua alikuwa ameiba.

Baba : Unajua ni hatia kuwa na simu tamba shuleni na kuwa na mali ya kuiba?

Mwana : (Akiogopa) Nisamehe baba.

Baba : (Akitikisa kichwa)Sasa imekuwaje ?

Mwana : (Kwa mkono unaotetema)Mwalimu mkuu amenituma nyumbani na kunipa barua hii nikuletee.

Baba : ( Akiipokea , kuifungua na kuisoma barua) Kesho tutaandamana hadi shuleni.

Tazama video hii.
Michezo ya kuigiza huwa na umuhimu gani katika jamii?

i) kuburudisha
ii) kufunza
iii) kuadilisha
iv) kukuza vipawa vya wasanii
v) kutafakirisha
vi) kuliwaza
vii) kuonya na kutahadharisha
viii) kuhamasisha
ix) njia ya kujipata riziki
x) hukuza staid za lugha
xi) kustawisha utamaduni
xii) kukuza umoja

Utungaji wa mchezo wa kuigiza huzingatia kaida zifuatazo:
i) kuteua mada ya kutungia
ii) kutumia lugha yenye mnato na mchomo ya hisia wa kutumia tamathali za usemi zinazokubalika kama tasifida, mafumbo, chuku, taharuki
iii) kuchagua mandhari yafaayo
iv) kuzingatia ufaafu wa waigizaji
v) kuchagua maleba yatakayoafiki nafasi na hadhi za waigizaji
vi) kugawa mchezo katika maonyesho mbalimbali kulingana na mtiririko wa matukio

Order this CD Today to Experience the Full Multimedia State of the Art Technology!

For Best results INSTALL Adobe Flash Player Version 16 to play the interactive content in your computer. Test the Sample e-Content link below to find out if you have Adobe Flash in your computer.

Sample Coursework e-Content CD

Other Goodies for KCSE ONLINE Members!

Coursework e-Content CD covers all the topics for a particular class per year and costs 1200/- ( Per Subject per Class ).

Purchase Online and have the CD sent to your nearest Parcel Service. Pay the amount to Patrick 0721806317 by M-PESA then provide your address for delivery of the Parcel. Alternatively, you can use BUY GOODS TILL NUMBER 827208 Ask for clarification if you get stuck.

Install ADOBE Flash Player for Best Results

For Best results INSTALL Adobe Flash Player Version 16 to play the interactive content in your computer. Test the link below to find out if you have Adobe Flash in your computer.

Search

Subject Menu